Thursday, October 20, 2011

Vijana jitaabisheni kuzifahamu Sakramenti za Kanisa: mwanzo, uponyaji, ushirika na huduma!

Mpendwa kijana, uchambuzi wetu wa Katekismu ya Vijana, YOUCAT, unatuingiza katika kuzichanganua Sakramenti Saba za Kanisa.
Kwa ujumla Sakramenti za Kanisa zinaweza kupangwa katika makundi makuu matatu. Kundi la kwanza ni la Sakramenti za Mwanzo, ambazo zinamwingiza mtu katika kupokea imani. Sakramenti za kundi hili ni tatu: Ubatizo, Kipaimara na Ekaristi Takatifu. Kundi la pili lina Sakramenti za Uponyaji: yaani Kitubio na Mpako wa Wagonjwa. Na kundi la tatu ni la Sakramenti za Ushirika na Huduma: hizi ni sakramenti ya Ndoa na Madaraja Matakatifu.
SAKRAMENTI YA UBATIZO ni sakramenti ya msingi na ufunguo wa sakramenti zote, ni agano ambalo mtu hanabudi kulikubali; ni njia ya kutoka katika ufamle wa mauti kuingia uzimani; na ni mwanzo wa muungano dumifu na Mungu. Ubatizo unaweza kufanyika kwa kumzamisha mtu mara tatu ndani ya maji au kwa kummwagiliwa maji kichwani mara tatu huku kukitamkwa “F… nakubatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.” Maji ya Ubatizo yanawakilisha maisha mapya na kutakatifuzwa katika Kristo. Ibada ya ubatizo hufungwa kwa kupakwa mafuta matakatifu, vazi jeupe na mshumaa wa ubatizo. Ubatizo unatolewa kwa mtu yeyote ambaye hajabatizwa.
Hitaji la lazima ili kubatizwa ni imani ambayo mtu anaiungama hadharani wakati wa ubatizo. Ubatizo hutolewa pia kwa watoto wachanga ambapo ungamo la imani hufanywa na wazazi kwa niaba ya watoto hao. Ukweli ni kwamba kabla mtu hajaitikiwa wito wa kubatizwa Mungu tayari amekwisha mkubali kuwa miongoni mwa watoto wake.
Na hivyo ubatizo ni neema, ni zawadi tusiyoistahili toka kwa Mungu. Kukubali Ubatizo wa mtoto mchanga kwa wazazi waamini ni tendo la upendo na matashi mema ya kumnasua toka dhambi ya asili na nguvu ya mauti. Mtu yeyote anapobatizwa anakuwa mshirika wa Mwili wa Kristo, kaka na dada wa Mwokozi, na mwana wa Mungu.
Kwa mtu yeyote aliyepokea Injili na kufahamu kuwa Kristo ni “njia, na kweli na uzima” (Yoh 14:6), Ubatizo ni njia pekee ya kwenda kwa Mungu na ya wokovu. Hata hivyo, kwa vile Kristo alikufa kwa ajili ya watu wote, wale wote ambao hawajapata nafasi ya kujifunza kumhusu Kristo na imani lakini wanamtafuta Mungu kwa dhamiri zao wanapata wokovu kwa ubatizo wa tamaa.
Kwa kawaida, Sakramenti ya Ubatizo huadhimishwa na Askofu, Padre au Shemesi. Lakini katika hatari ya kifo kila mkristo au mtu yeyote (hata asiye mkristo) naweza kubatiza kwa kutumia maji na kutamka maneno ya ubatizo: “F. Nakubatiza kwa Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu”. Anayebatiza hana budi kuwa na nia ya kutenda kile kinachofanywa na Kanisa linapobatiza.
Katika Ubatizo mtu hupokea jina jipya ikionesha kwamba Mungu mwenyewe amemuita kwa jina, anamfahamu, na hivyo ni wake. (Is 43:1). Mkristo huchagua jina la watakatifu ili kijipatia mfano wa kuigwa na kupata msaidizi, rafiki aliye kwa Mungu.
SAKRAMENTI YA KIPAIMARA inakamilisha ubatizo kwa kumpatia mwimarishwa zawadi ya Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono; na kwa kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma anapata nguvu ya kutoa ushuhuda wa upendo na uwezo wa Mungu kwa maneno na matendo. Mwimarishwa anakuwa mshirika kamili na mwajibikaji wa Kanisa Katoliki.
Katika Agano la Kale, watu walisubiri ujio wa Roho Mtakatifu juu ya Masiha. Na katika maisha yake, Kristo ameonesha kuwa na Roho wa upendo na muungano kamilifu na Baba. Huyu ndiye Roho aliyesubiriwa katika Agano la Kale, na ambaye Kristo aliwaahidia wafuasi wake; ndiye aliyewashukia wafuasi wake siku ya Pentekoste, na anayemshukia kila mmoja apateye Kipaimara.
Kinachofanyika wakati wa Kipaimara ni kwamba roho ya mkristo mbatizwa inapata muhuri usiofutika na unaomtambulisha mtu kuwa mkristo daima. Paji la Roho Mtakatifu linamwimarisha mtu kuwa shuhuda wa Kristo kwa maneno na matendo kupitia neema ya ubatizo.
Kipaimara kinaweza tu kutolewa kwa Mkristo Mkatoliki aliyebatizwa na aliye katika hali ya neema, yaani asiwe katika dhambi ya mauti. Kama mtu ametengana na Mungu kwa dhambi kubwa anapaswa kujipatanisha naye kwa kupokea Sakramenti ya kitubio. Sakramenti ya Kitubio inahitajika pia katika mazingira yote ambapo mtu anahitaji kujipatanisha na nafsi yake, na watu wengine, na Mungu, na kumkaribia Mungu hata kama hajatenda dhambi ya mauti.
Mwadhimishaji wa kawaida wa Sakramenti ya Kipaimara ni ASKOFU. Hata hivyo kama kuna sababu nzito na za lazima, Askofu anaweza kumruhusu padre atoe Kipaimara. Kunapokuwa na hatari ya kifo, padre yeyote anaweza kutoa kipaimara.
Kwa leo mpendwa kijana, naomba tukunje jamvi letu ili tuweze kujipatia muda wa kucheua haya tuliyopokea. Uchambuzi wetu wa Sakramenti saba za kanisa utaendelea wiki ijayo, siku na wakati kama huu. Nikikutakia kila jema, kutoka hapa Vatican, ni mtumishi wako, Padre Flavian Kassala.SOURCE kutokahttp://www.radiovaticana.org/EN3/articolo.asp?c=504225

1 comment:

  1. Sakramenti ni muhimu sana kwa safari yetu hapa duniani....maana wengi wetu tumekuwa tunadharau kushiriki sakramenti hasa Kitubio tukijifariji kwamba ya nini nikaungame kwa Padri?si sawa....na hata kwenda kujongea altare ya Bwana kwa vijana imekuwa issue vikwazo haviishi...uchumba gani tunaokumbatia.......

    ReplyDelete