B.Maria

Sisi Wakatoliki nyakati hizi zilizojaa madhehebu mbalimbali ya Kikristo, yanayotumia Biblia na kuitafsiri kadiri ya
imani yao ama wenyewe wanavyojisikia kwa namna fulani, tunajikuta tukichanganyikiwa na pengine kuona aibu ya
kumheshimu Mama Bikira Maria. Tunapoanza kuchunguza nafasi yake katika fumbo la ukombozi wa mwanadamu,
tunakiri pamoja naye kuwa ni Mwenyezi Mungu aliyemtendea makuu (Lk 1:49). Halafu tunakiri kwa unyenyekevu
wote pamoja na Yohane Mbatizaji, “Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu” (Yoh 3:27). Hivyo yale yote
tunayoyasadiki kuhusu Bikira Maria, hakujipatia mwenyewe bali amejaliwa na Mwenyezi Mungu na kuitikia kwa
hiari fumbo la mpango wake.
MAANDIKO YANASHUHUDIA UMUHIMU WA WATU UNAOTOFAUTIANA
Maandiko matakatifu yanawasifu watu mbalimbali kutokana na walivyomuamini Mungu na kutenda makuu kwa
ajili ya taifa lake. Abrahamu alimuamini na kuwa tayari kumtolea sadaka mwanae Isaka, tukio lililomfanya apate
baraka ya pekee ya kuwa baba wa waamini (Mwa 22:15-18). Yosefu, kipenzi wa Yakobo, alikuwa mwaminifu hata
akaliokoa taifa lisiangamie kwa njaa (Mwa 50:20). Musa ndiye mkombozi wa taifa la Mungu katika Agano la Kale:
aliongoza Israeli kutoka utumwani Misri akalipatia sheria kutoka kwa Mungu katika mlima Sinai. Maandiko ya
Agano la Kale yanakiri, “Wala hajainuka kiongozi kama alivyokuwa Musa” (Kumb 34:10-12). Kwa kuwa watu hao ni
wengi mno tunaorodhesha wafuatao: Yoshua, Debora, Gideoni, Samsoni, Samweli, Ruthu, wafalme Daudi na
Solomoni, manabii Eliya, Yeremia na Ezekieli. Nabii Isaya ana sifa ya pekee katika kumchora Masiya. Mwishoni
Bwana Yesu mwenyewe anamsifu Yohane Mbatizaji akisema, “Ni mkuu kati ya uzao wa wanawake” (Lk 7:24-28).
Bikira Maria ana nafasi gani kati yao? Hao tuliowataja walitenda kweli mambo makuu kwa imani, lakini Bikira
Maria yuko juu sana kupita hao wote, tena kwa mbali: yeye ni malkia wa makundi yote ya mbinguni, sio ya watu
tu, bali hata ya malaika. Mapokeo ya mashariki humuita “daraja linalounganisha dunia na mbingu”, “mfano
aliouona Yakobo” (Mwa 28:12).
BIKIRA MARIA KATIKA BIBLIA
UTABIRI KUHUSU BIKIRA MARIA, EVA MPYA
Mapokeo yamtazama Bikira Maria kama Eva mpya atakayemshinda nyoka wa kale (Ibilisi). Kwa nini Eva mpya?
Kwa sababu Eva wa kale alidanganywa na kuangushwa na Shetani, hivyo alitenda dhambi. Kumbe Maandiko
matakatifu yanatupatia utabiri kuhusu Eva mpya atakayemshinda adui (Shetani) kwa kumponda kichwa: “Nitaweka
uadui kati yako na huyu mwanamke, kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa chako” (Mwa 3:15).
“Tazama Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamuita jina lake Emanueli, yaani Mungu
pamoja nasi” (Isa 7:14). Dondoo hilo lilinganishwe na Lk 1:34-35, “Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje
neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu akakujilia juu yako, na nguvu zake
Aliye juu zitakufunika kama kivuli. Kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”.
Utabiri mwingine wasema, “Litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa
matunda. Na Roho wa Bwana atakaa juu yake, Roho ya hekima na ufahamu, Roho wa shauri na uwezo, Roho wa
maarifa na ya kumcha Bwana” (Isa 11:1-2). Je, shina hilo si yeye Mama Bikira Maria, na tawi alilochipusha si
Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo?
“Umebarikiwa wewe katika kila hema la Yuda na katika kila taifa, nao wanaposikia jina lako watafadhaika.
Imani yako haitatoka mioyoni mwa watu wanaoukumbuka uweza wa Mungu milele” (Yudithi 14:7; 15:9).
Linganisha dondoo hili na Lk 1:42, “Akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe kuliko wanawake wote,
na yeye utakayemzaa amebarikiwa”. Je, utasema Bikira Maria ni mtu wa ziada katika mpango wa Mungu?
Tena tunasoma, “Imba, ee binti Sion, piga kelele, ee Israeli, furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, ee binti
Yerusalemu. Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana yu katikati yako” (Sef 3:14-15). Linganisha dondoo hilo na
Injili: “Malaika akaingia nyumbani mwake akamwambia, Furahi Maria, umejaliwa neema kubwa, Bwana yu pamoja
nawe” (Lk 1:28).
BIKIRA MARIA KATIKA AGANO JIPYA
Mambo yaliyotabiriwa katika Agano la Kale yametimia katika Agano Jipya: ukombozi wetu ulianza pale Bikira
Maria alipokubali fumbo la umwilisho wa Mwana wa Mungu, akisema kwa hiari, “Mimi ni mtumishi wa Bwana, na
iwe kwangu kama ulivyonena” (Lk 1:38).
Je, Bikira Maria ni bahasha? Siku hizi kuna baadhi ya waheshimiwa ambao wanadhani kujua Maandiko kuliko
watu wengine, tena wanadai wanaye Roho Mtakatifu; kumbe wanadiriki kumuita Mama huyo mtakatifu, eti ni
“bahasha” ambayo ikileta barua haina kazi! Jambo hili linasikitisha sana na sio tu kumkosea heshima Mama yetu
mpendwa wa mbinguni, bali inaweza pia kuwa kufuru kwa Mwenyezi Mungu aliyemuumba kama msaidizi wa
Mkombozi aliyejaa neema.
Manabii mbalimbali kwa mwanga wa Roho Mtakatifu walimuagua kwa heshima; Mama Elizabeti alijiona hastahili
kutembelewa naye akamuita, “Mama wa Bwana wangu”; mzee Simeoni alimuagulia mateso yenye uchungu kama
upanga yatakayopenya moyowe. Bwana Yesu aliyefurika Roho Mtakatifu tangu nukta ya kuchukuliwa mimba,
wakati alipokaribia kufa pale msalabani alimuita, “Mama”; jumuia ya Mitume na wafuasi wa kwanza walimtaja
kipekee ilivyo ishara ya heshima. Je, Roho Mtakatifu ndiye anayewaongoza hawa ndugu zetu wamuite bahasha? Je,
ni Roho yuleyule aliyewaongoza Mitume na manabii ama roho ya aina nyingine? “Wapenzi wangu, msisadiki kila
mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa
Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni” (1Yoh 4:1).
Bikira Maria sio “chombo” tu, bali mshiriki wa kazi ya ukombozi ya Mwanae. Kadiri ya mtume Paulo kuteseka ni
kutimiliza yaliyopungua katika mateso ya Kristo kwa ajili ya Kanisa, “Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu,
maana kwa mateso yangu hapa duniani nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo” (Kol
1:24). “... maana tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake” (Rom 8:17b). Katika hilo la
kumfuata Mwanae katika mateso Bikira Maria alitabiriwa wazi na mzee Simeoni, “Tazama huyu amewekwa kwa
kuanguka na kuinuka wengi katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe uchungu ulio kama
upanga utauchoma moyo wako” (Lk 2:34-35).
Bikira Maria alishiriki mateso ya ukimbizi huko Misri kwa lengo la kumficha Mwanae asiteswe na Herode, “Hivyo
Yosefu aliamka akamchukua mtoto pamoja na Mama yake akaondoka usiku akaenda Misri akakaa huko mpaka
Herode alipokufa” (Math 2:14-15).
BIKIRA MARIA MWOMBEZI KATIKA HARUSI YA KANA: Mama Bikira Maria anaonekana mwenye kuonea
huruma wenye shida: kwa ombi lake huko Kana ya Galilaya Yesu aligeuza maji kuwa divai, na wanafunzi wake
wakamwamini (Yoh 2:1-12).
BIKIRA MARIA AFANYWA EVA MPYA: Juu ya Eva wa zamani imesemwa ni Mama wa walio hai: “Adamu
akamwita mkewe jina lake Hawa, kwa kuwa ndiye aliye Mama wa walio hai” (Mwa 3:20). Hata hivyo Agano Jipya
linaonyesha Adamu na Eva wa zamani wametuletea kifo (Rom 5:12).
Yesu, aliye Adamu mpya, alipokuwa anakamilisha sadaka ya ukombozi pale msalabani alimfanya Bikira Maria
awe Eva mpya kwa kitendo cha kumkabidhi mwanafunzi, tena yule aliyempenda zaidi. “Basi Yesu aipomwona
Mama yake na yule mwanafunzi aliyempenda amesiMama karibu akamwambia Mama yake, Mama, tazama
Mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama Mama yako” (Yoh 19:26-27). Zaburi yasema, “Lakini juu
ya Sion itasemwa, Sion ni Mama yao wote; Mungu mkuu ameuthibitisha. Mwenyezi Mungu ataorodhesha mataifa
na kuandika juu ya kila moja, Huyu chanzo chake ni Sion” (Zab 87:5-6).
Pale msalabani Bikira Maria:
• alifanywa Mama wa wote wanaompenda Mwanae;
• alifanywa malkia wa wafiadini;
• kisha kumzaa pasipo uchungu Bwana wa uzima, pale alituzaa sisi kwa uchungu wa kutisha uliotokana na
kumuona Mwanae akifa msalabani. Hata hivyo Bikira Maria aliendelea kumuamini Mwanae aliyeonekana
ameshindwa;
• katika kuteswa kwa Yesu Bikira Maria alishuhudia hatua kwa hatua; wanafunzi wa Yesu walipokimbia na
kumtazama kwa mbali, Bikira mtakatifu alikuwa karibu akaona vema kila teso lililompata. Tena
kutokana na fungamano la upendo wa ajabu lililokuwepo kati ya Yesu na Mamaye, aliposhuhudia mateso
ya Mwanae aliteseka sana katika moyo wake safi usio na doa, kiasi kwamba baadhi ya watakatifu
wanasema, Msalaba wa Yesu uliwasulubisha wote, Yesu mwilini na Mama yake moyoni. Uaguzi wa mzee
Simeoni ulitimia hivyo.
JE, BIKIRA MARIA ALIZAA WATOTO WENGINE?
Mapokeo kuhusu Bikira Maria yanaonyesha alikuwa binti pekee wa wazee watakatifu Yohakimu na Ana. Vilevile
Mt. Yosefu, ingawa kisheria alikuwa mume wake, hakutenda naye tendo la ndoa hata moja. Ndiyo maana kwenye
litania yake tunamuita mwenye usafi kamili. Alikufa kabla Yesu hajaanza utume kwa kubatizwa kwenye mto
Yordani. Sisi tunasadiki Maria ni “Bikira daima”.
Ndugu wa Yesu wanaosemwa katika Injili ni kina nani? Wanaosemwa katika Injili “ndugu zake Yesu” si watoto
wa Bikira Maria wala Yosefu mtakatifu, bali ndugu wa kiukoo waliokuwa jirani sana na familia hiyo takatifu. Kama
Bikira Maria angekuwa na watoto wengine, je, Yesu Bwana wetu asingekuwa amefanya kosa la kiudugu
kuwanyang’anya Mama yao na kumfanya awe Mama wa mtume Yohane alipomkabidhi msalabani, “‘Mwana, tazama
Mama yako’. Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake” (Yoh 19:27).
Katika Agano Jipya yupo Yakobo anayeitwa na mtume Paulo “ndugu yake Bwana” (Gal 1:19): Yakobo huyo
alikuwa maarufu katika Kanisa la Yerusalemu (Mdo 12:7; 15:13-21; 21:18-20; Gal 2:9). Yakobo huyo si mtume
Yakobo mwana wa Alfayo, wala mtume Yakobo kaka yake Yohane (Lk 6:12-16), bali ni Yakobo ndugu yake Yose na
mama yao kwenye Injili anaitwa “Maria mwingine”, si Maria Mama wa Yesu. “Walikuwepo pia wanawake
waliotazama kwa mbali. Miongoni mwao akiwa Maria Magdalena, Salome na Maria mama wa akina Yakobo mdogo
na Yose” (Mk 15:40). Maria lilikuwa jina la kawaida kwa Wayahudi: akina Maria wakiwa wengi hivyo, tujue
kuwatofautisha kwenye Injili. Bikira Maria Injili zinamtaja kama “Mama wa Yesu”.
JE, WAKATI WA KUFANYA UTUME YESU ALIMDHARAU MAMA YAKE?
Wengine husoma Maandiko matakatifu wakiishia ujuu bila ya kufikiria wala kulinganisha na mistari mingine.
Hivyo hukwazwa na semi kadhaa za Bwana Yesu ambazo kimsingi hazimpingi Mama yake, bali zinampongeza.
“Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu akasema, ‘Hongera kwa mwanamke
aliyekuzaa na kukunyonyesha’. Yesu akamjibu, ‘Barabara, lakini heri yake zaidi yule anayelisikia Neno la Mungu na
kulishika’” (Mk 11:27-28).
Tena lingine lasema, “Basi, mtu mmoja akamwambia, ‘Mama yako na ndugu zako wako nje, wataka kusema
nawe’. Lakini Yesu akamjibu huyo mtu aliyemwambia hivyo, ‘Mama yangu ni nani, na ndugu zangu ni akina nani?’
Kisha akanyosha mkono wake juu y aweanafunzi wake akasema, ‘Hawa ndio Mama yangu na ndugu zangu, maana
yeyote anayefanya anavyotaka Baba yangu aliye mbinguni, huyo ndiye kaka yangu na dada yangu na Mama
yangu’” (Math 12:46-50).
Je, sehemu hizi za Maandiko zinampinga kweli Bikira Maria au zinampongeza? Sababu:
• Jamaa yake Elizabeti alimpongeza, tena akiongozwa na Roho Mtakatifu, “Heri yako wewe uliyesadiki
kwamba yatatimia yale uliyoambiwa na Bwana” (Lk 1:45).
• Bikira mtakatifu alipopashwa habari na malaika hakukataa mpango wa Mungu, bali kwa hiari yake
alikubali fumbo la mpango wake. “Maria akasema, ‘Mimi ni mtumishi wa Bwana, na iwe kwangu kama
ulivyonena’. Kisha malaika yule akaenda zake” (Lk 1:38).
• Bwana Yesu alitaka kuwainua wasikilizaji wake wafuate mambo ya Kiroho kuliko ya mwilini. Hivyo ni
kweli, Bikira Maria anasifiwa kwanza kwa imani yake, iliyokuwa ya juu zaidi kushinda hata ile ya
Abrahamu, kuliko kwa kumchukua Yesu tumboni tu. Hata hivyo tusisahau kuwa Yesu, kama mtu yeyote
mcha Mungu, aliwaheshimu wazazi wake, tena tunasikia aliwatii. “Basi, akarudi pamoja nao Nazareti,
akawa anawatii” (Lk 2:51).
Naomba, kabla hujahukumu neno moja, angalia ujumla wake.
Yesu alizaliwa na Bikira mtakatifu, ndiye aliyemlea na kuhangaika naye huko na huko hata Misri ili kumuepusha
na kifo. Ishara ya kwanza kwenye maisha ya hadhara iliyongozwa na Bikira Maria huko Kana. Maria alikuwepo hata
wakati wa Yesu kuteswa, akiteseka pamoja naye. Pale msalabani alikabidhiwa Kanisa kwa njia ya Yohane mtume.
Bikira Maria alikuwepo hapo mwanzo wa Kanisa, na ndiye aliyelivutia zaidi Roho Mtakatifu kwa njia ya sala yake.
“Hao wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria Mama yake Yesu na
ndugu zake” (Mdo 1:14).
DOGMA ZA KANISA KUHUSU BIKIRA MARIA
Kuna mafundisho makuu manne kumhusu Bikira Maria ambayo ni lazima kila Mkatoliki ayasadiki kutokana na
ufunuo wa Mungu:
1. B. Maria mkingiwa dhambi ya asili
2. B. Maria Mama wa Mungu
3. B. Maria Bikira daima
4. B. Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho
MKINGIWA DHAMBI YA ASILI
Tunasadiki Bikira Maria tangu atungwe mimba Mungu alimkinga na kila doa la dhambi kwa kutazamia stahili za
Yesu Kristo aliye Mkombozi wa binadamu wote. Ndiye mwanakanisa aliyekombolewa kwa namna bora kushinda
viungo vyote vya Kanisa. Maisha yake yote hakutenda dhambi hata moja. Mapokeo ya mashariki yanamuita A
Panagia = Mtakatifu tu. Dogma hiyo ilitangazwa na papa Pius IX mwaka 1854, hata mwaka 1858 Bikira Maria
alijitambulisha huko Lurdi (Ufaransa) kwa Mt. Bernadetta Soubirous kama Mkingiwa. Tena pale Fatima (Ureno)
tumefunuliwa moyo wake safi usio na doa.
MAMA WA MUNGU
Injili ya Yohane inaanza kwa kishindo, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu,
naye Neno alikuwa Mungu” (Yoh 1:1). Huyo Mungu Mwana ndiye aliyetwaa ubinadamu katika Bikira Maria
akazaliwa mtoto, jina lake Yesu, maana yake Mungu Mwokozi. Huyo ni binadamu kama sisi isipokuwa hana
dhambi. Ubinadamu wa Yesu unategemea Nafsi yake ya Kimungu, hivyo akisema, ‘Mimi’, anamaanisha Nafsi yake
ya Kimungu. Ndiyo maana aliwaambia Wayahudi, “Kweli nawaambia, kabla Abrahamu hajazaliwa, nalikuwepo”
(Yoh 8:50). “Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo alivyomjalia Mwanae kuwa asili ya uhai” (Yoh 5:26).
Je, Bikira Maria ni Mama wa Mungu tangu lini? Mtume Paulo anaeleza, “Wakati maalumu ulipotimia Mungu
alimtuma Mwanae aliyezaliwa na mwanamke” (Gal 4:4). Ni kwanzia wakati huo: sasa imepita miaka 2006 tangu
Bikira Maria ajiliwe na sifa hiyo ya kumchukua mimba, kumzaa, kumnyonyesha na kumlea mtu ambaye kwa asili ni
Mungu. Cheo hicho kimemuinua juu kuliko hata malaika, akawa malkia wao. “Malaika alimwambia, ‘Hicho
kitakachozaliwa kitaitwa Kitakatifu, Mwana wa Mungu’” (Lk 1:35). Dogma ilitolewa mwaka 431 kwenye Mtaguso wa
Efeso uliomuita “Mzazi wa Mungu”.
BIKIRA NA MAMA
Fumbo la Bikira Maria hapa linagongana na akili ya kibinadamu. Wote wanakiri ya kuwa Yesu alimwilishwa bila
ya mchango wa mwanamume, kumbe la ajabu zaidi ni kwamba hata uzazi wenyewe haukuondoa ubikira wake, bali
uliutakasa. Ingawa akili yetu inakataa, sisi tunakiri na malaika, “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu” (Lk 1:38).
Ndiyo maana tunamkiri ni Bikira daima.
KUPALIZWA MBINGUNI MWII NA ROHO
Baada ya maisha haya ya duniani Bikira Maria mwenye heri alipalizwa mbinguni mwili na roho, ishara ya
mwanamke mshindi. “Ishara kubwa ikaonekana mbinguni, ambapo mwanamke aliyevikwa jua, pia na mwezi chini
ya miguu yake, na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake” (Ufu 12:1).
HESHIMA ZA LITURUJIA KWA MARIA
Kuna ibada za Mama Bikira Maria zinazoadhimishwa katika liturujia. Hapa tunazipanga kulingana na heshima
zinavyozidiana:
SHEREHE
8 Desemba – Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
1 Januari – Bikira Maria Mama wa Mungu
25 Machi – Bikira Maria Kupashwa Habari
15 Agosti – Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni
SIKUKUU
31 Mei – Maamkio ya Bikira Maria
8 Septemba – Kuzaliwa kwa Bikira Maria
KUMBUKUMBU
Juni – Moyo Safi wa Maria
15 Septemba – Mama Yetu wa Huzuni
22 Agosti – Bikira Maria Malkia
7 Oktoba – Bikira Maria wa Rozari
21 Novemba – Bikira Maria Kutolewa Hekaluni
KUMBUKUMBU YA HIARI
11 Februari – Mama Yetu wa Lurdi
16 Julai – Mama Yetu wa Mlima Karmeli
5 Agosti – Kutabaruku wa Kanisa la B. Maria
Tena kila Jumamosi isiyo na adhimisho maalumu, Kanisa huadhimisha kumbukumbu ya Mama wa Mungu.
Pia zipo heshima za binafsi kwa Bikira Maria mwenye heri: mashariki tenzi na nyimbo (k.mf. Akatistos, tenzi za
mt. Efrem shemasi, na nyingine); magharibi (Roma) tunamheshimu binafsi na hata kijumuia kwa kusali rozari
takatifu. Ndiyo ibada ya binafsi inayompendeza sana baada ya zile za liturujia hata akatokea sehemu mbalimbali
duniani akihimiza tusali rozari ili tupate amani binafsi, kitaifa na kimataifa. Mwezi wa tano ni mwezi wa Maria.
Mwezi wa kumi ni mwezi wa Rozari. Mtu aliyeonja matunda ya kumheshimu Maria mtakatifu, Mama wa Mungu,
anajua uwezo wa maombezi yake. Kanisa linakiri neema zote za Mungu zaja kwetu kwa njia ya Maria.
Je, tunamuabudu Bikira Maria? Hapana, Bikira Maria hatumuabudu hata kidogo, bali tunamtolea heshima ya juu
kuliko watakatifu wengine. Mungu tu tunampa heshima ya ‘latria’ (kuabudu), watakatifu tunawaheshimu (dulia) na
Bikira Maria tunampa heshima sana (yuper-dulia).
Kweli Mama Bikira Maria ni “kina kisichochunguzika kwa macho ya malaika” (Akatistos). Ni fumbo la ajabu
alilolifanya Mungu katika mpango wa wokovu kwa ajili yake na kwa ajili yetu. Katika Injili ya Yohane Bwana Yesu
alisema, “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili, lakini atakapokuja huyo Roho
wa ukweli atawaongoza kwenye ukweli wote” (Yoh 16:12-13). Kwa msaada wa Roho Mtakatifu heshima kwa Bikira
Maria ilienea katika Kanisa lote tangu zamani kabisa. Tena katika Injili ya Luka kuna utabiri wa kumheshimu Bikira
Maria vizazi vyote, “Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mdogo, hivyo tangu sasa vizazi vyote
wataniita mwenye heri” (Lk 1:48).