NEWS


UDANGANYIFU katika mitihani nchini umeanza kushika kasi baada ya jana Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kutangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza sekondari mwaka jana, ambao watahiniwa 3,303 wamebainika kuufanya kwa zaidi ya mara 10 ya mwaka juzi. 

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa hao, ambao kati yao, 3,301 ni wa Mtihani wa Kidato cha Nne na wawili ni wa Maarifa (QT). Mwaka juzi, wanafunzi 303 walibainika kufanya udanganyifu huo. Aidha, watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 wamefaulu mtihani wa huo, wakiwamo wasichana 90,885 sawa na asilimia 48.25 ya wasichana waliofanya mtihani na wavulana ni 134,241 sawa na asilimia 57.51 ya wavulana waliofanya mtihani huo.
 

Mwaka juzi, watahiniwa waliofaulu walikuwa 177,021 sawa na asilimia 50.40 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo, hivyo kiwango cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 2.63. Dk. Ndalichako alifafanua aina ya udanganyifu wa watahiniwa hao na kusema zaidi ni 2,896 wamefutiwa matokeo kwa sababu ya kuwa na mfanano wa majibu usio wa kawaida. Alisema wadanganyifu wengi wanatoka Mwanza na Arusha.
 

Alizitaja aina nyingine za udanganyifu na idadi ya watahiniwa waliohusika kwenye mabano, kuwa ni waliokamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mitihani wakiwa na ‘notes’ (182); waliofanyiwa mitihani na watu wengine (3); waliosajiliwa kufanya mitihani kwa kutumia majina ya wengine wakati walishafanya mtihani (4) na waliokuwa na karatasi za majibu zenye miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti katika karatasi ya somo moja (155).
 

Nyingine ni kubadilishana karatasi za maswali/vijitabu vya kujibia mtihani ili kuandikiana majibu, au kujadiliana ndani ya chumba cha mtihani (14); watahiniwa kukamatwa na booklet zaidi ya moja ambapo booklet moja hawakupewa na msimamizi (18) na watahiniwa kubainika kuwa na kesi mbili tofauti; kama vile mfanano wa majibu, notes, kijitabu cha kujibia zaidi ya kimoja na kubadilishana karatasi za majibu au kijitabu cha kujibia mtihani (25).
 

“Wapo wengine watatu ambao walikamatwa wakifanyiwa mitihani na mmoja aliyekuwa akiwafanyia mitihani ni wa kidato cha tatu ambaye mwaka huu anaingia kidato cha nne. Sasa unajiuliza kama huyo ameanza udanganyifu huo, kwa kweli ni hatari,” alisema. Dk. Ndalichako alisema pia wapo waliobainika kukosa sifa za kufanya uchaguzi miaka ya nyuma na kurudia
 
na wanafunzi wanne wa Kahama Muslim, waligundulika kwa hilo kwa kuangalia picha zilizotumika mwaka 2010.
 

Kuhusu mfanano wa majibu, alisema “mwaka jana, tulipotangaza matokeo ya darasa la saba na kubainisha udanganyifu na kufuta matokeo, wapo waliotushutumu sana na mimi niliamua kukaa kimya. Wapo waliodai ni kwa sababu tunatunga mtihani wa maswali ya kuchagua na usimamizi holela.” Lakini alisema wanafunzi wana uwezo tofauti darasani, hata kama watafundishwa na mwalimu mmoja, hivyo si rahisi kwa majibu ya darasa zima kufanana hata katika maswali ya kuchagua na katika kuandika maswali ya kujieleza, kukokotoa Hisabati; ambako kote huko wanafunzi hawawezi kufafana kwa jibu sahihi wala njia walizotumia kupata jibu; hali ambayo alisema imejitokeza katika majibu ya watahiniwa 2,896.
 

“Kwa mfano, kuna kituo wanafunzi wote 50 walijaza jibu la kuchagua linalofanana lakini wamekosa, hii si kawaida. Katika somo la Jiografia, kuna kituo wanafunzi wote walijaza jibu la O wakati hakukuwa na jibu hilo. Kwa upande wa waliobadilishana karatasi, walikuwa 14 akiwamo mmoja ambaye aliandika kwenye kitambulisho chake, ‘Kwa Mage’ na mwenzake akamjibu ‘Haisomeki’. Aandika mistari Bongofleva Kuhusu walioandika mambo yasiyoeleweka, alisema yupo mwanafunzi aliyeandika mashairi ya muziki wa kizazi kipya, - Bongofleva, na mwingine kuchora mchezaji anayesakata soka.
 

Lakini pia wapo wanane walioandika matusi akiwamo mmoja aliyeandika matusi katika mitihani yake yote saba. Baadhi ya mistari aliyosoma mtendaji huyo wa Necta iliyoandikwa na mtahiniwa aliyejibu kwa kuandika Bongofleva ni “wakati majibu yakitoka nitakuwa mtaani, wazazi wangu wako levo ya juu…hii ndio yangu time.” Kwa walioandika matusi, alisema kufuta matokeo pekee hakutoshi, hivyo Necta itafuatilia zaidi na kuchukua hatua ikiwamo kufikishwa katika vyombo vya sheria, kwa sababu ni kosa kisheria na kuwataka wanafunzi ambao hawawezi kujibu maswali, waandike namba zao tu na kukusanya karatasi, badala ya kutukana.
 

“Kwa kweli hali hii ni hatari. Taifa linaangamia, tunajichimbia kaburi wenyewe. Hili si tatizo la Baraza la Mitihani, ni la Taifa zima. Linahusu wazazi, walimu na wanafunzi wenyewe na jamii yote kushirikiana kukomesha tabia hii,” alieleza Dk. Ndalichako ambaye kitaaluma ni
 
mwalimu. Alisema kufuta matokeo pekee hakutoshi, kwa sababu inaonekana wapo watu waliojitengenezea ajira, kwani ushahidi unaonesha wapo walioshiriki udanganyifu huo tangu
 
mwaka 2009 hadi mwaka jana, kwa kuwajazia wanafunzi majibu, hivyo hatua za kisheria ni lazima zichukuliwe.
 

“Watahiniwa wote waliofutiwa matokeo yao kutokana na kujihusisha na udanganyifu au kuandika matusi kwenye karatasi zao za majibu, hawataruhusiwa kufanya Mtihani wa Baraza kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu,” alieleza Katibu Mtendaji wa Necta na kuongeza: “Kwa upande wa wasimamizi wote ambao vituo walivyosimamia vimebainika kuwa na watahiniwa wengi waliofanya udanganyifu, orodha yao itapelekwa kwa waajiri wao ili wachukuliwe hatua stahiki.
 

Aidha, mawasiliano yatafanyika pia na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuona hatua zaidi za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao,” alisema Dk. Ndalichako. Aidha, alisema Necta imesitisha matokeo ya watahiniwa 264 wa kujitegemea na 116 wa QT ambao walifanya mitihani bila kulipa ada, 873 wa shule binafsi ambao watatakiwa kulipa ada zao ili matokeo yao yafunguliwe, vinginevyo baada ya miaka miwili yatafutwa. Watahiniwa 67 hawajawasilisha alama zao za mazoezi.
 

Hata hivyo aliwataka wazazi kuacha kukimbilia kukata rufaa kama walivyofanya baadhi mkoani Morogoro kupinga hatua dhidi ya wanafunzi wa darasa la saba waliofutiwa matokeo mwaka jana, akisema wasubiri hali halisi itabainika wazi kwa ushahidi. Akifafanua matokeo, jumla ya watahiniwa wa shule 180,216 sawa na asilimia 53.59 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha nne wamefaulu; kati yao wakiwa ni wasichana 69,913 sawa na asilimia 44.36 na wavulana ni 110,303 sawa na asilimia 53.53.
 

Akizungumzia ubora wa ufaulu kwa jinsi, Katibu Mtendaji huyo alisema unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 33,577 sawa na asilimia 9.98 wamefaulu kwa madaraja ya kwanza hadi ya tatu; wasichana wakiwa 10,313 sawa na asilimia 7.13 na wavulana ni 23,264 sawa na asilimia 12.13. Mchanganuo unaonesha kuwa matokeo ya wavulana kwa madaraja ni la kwanza (2,571); la pili (5,658); la tatu (15,035); la nne (87,039) na waliopata sifuri ni 81,418.
 

Kwa wasichana kuanza daraja la kwanza ni 1,100; la pili 2,454; la tatu 6,759; la nne 59,600 na sifuri ni 74,667. Wanaoongoza Alizitaja shule 10 zilizofanya vyema katika kundi la shule zenye watahiniwa 40 na zaidi ni St. Francis Girls (Mbeya), Feza Boys (Dar), St. Joseph Millennium (Dar), Marian Girls (Pwani), Don Bosco (Iringa), Kasita Seminary (Morogoro), St. Mary’s Mazinde Juu (Tanga), Canossa (Dar), Mzumbe (Moro) na Ilboru (Arusha).
 

Kwa shule 10 za mwisho zenye watahiniwa 40 na zaidi ni Bwembwera, Pande Darajani, Mfundia, Zirai (Tanga), Kasokola (Rukwa), Tongoni (Tanga), Mofu, Mziha (Morogoro), Maneromango na Kibuta za Pwani. Aidha, shule 10 bora zenye watahiniwa chini ya 40 ni Thomas More Machrina (Dar), Feza Girls (Dar), Dung’unyi Seminary (Singida),
 
Maua Seminary (K’njaro), Rubya Seminary (Kagera), St. Joseph Kilocha Seminary (Iringa), Sengerema Seminary (Mwanza), Lumumba (Unguja), Queen of Apostles Ushirombo
 
(Shinyanga) na Bihawana Junior Seminary (Dodoma).
 

Shule goigoi katika kundi hilo ni Ndongosi, St Luke (Ruvuma), Igigwa, Kining’ila (Tabora), Ndaoya (Tanga), Kilangali (Moro), Kikulyungu (Lindi), Usunga (Tabora), Mtu Bubu Day (Dodoma) na Miguruwe (Lindi). Wanafunzi 10 bora ni Moses Swai (Feza Boys), Rosalyn Tandau (Marian Girls), Mboni Maumba (St Francis Girls, Mbeya), Sepiso Mwamwelo (St Francis Girls), Uwella Rubuga (Marian Girls), Hellen Mpanduji (St Mary’s Mazinde Juu), Daniel Maugo (St Joseph Millennium, Dar), Benjamin Tilubuzya (Thomas More Machrina, Dar), Simon Mbangalukela (St Joseph Millennium) na Nimrod Rutatora (Feza Boys).
 

Wasichana 10 bora ni Tandau (Marian), Maumba (St Francis), Mwamelo (St Francis), Rubuga (Marian), Mpanduji (Mazinde Juu), Lisa Chille (St Francis), Elizabeth Ng’imba (St Francis), Doris Noah (Kandoto, K’njaro), Herieth Machunda (St Francis) na Daisy Mugenyi (Kifungilo). Wavulana 10 bora ni Swai (Feza), Maugo (St Joseph Millennium), Tilubuzya (Thomas More Machrina), Mbangalukela (St Joseph Millennium), Rutatora (Feza), Simon Mnyele (Feza), Pascal Madukwa (Nyegezi Seminary), Henry Stanley (St Joseph Millennium), Fransisco Kibasa (Mzumbe) na Tumaini Charles (Ilboru).




Jumla Maoni (3)



Maoni

Haijapata kutokea wanafunzi waliofanya mtihani kutoka shuleni kuwa 180000 waliofaulu daraja la kwanza hadi la nne 34,000 waliopata sifuri ni 156, 000 

Hebu watanzania tujiulize tutafika kweli kwenye ulimwengu wa sayansi na teknologia
 

Nani alaumiwe hapa wanafunzi ,walimu, wazazi, wabunge,au serikali kwa ujumla. hili nalileta kama changamoto kwani inaumiza kwa wale wanaotaka maendeleo ya kweli
 

Hebu tusaidiane watanzania wenzangu kupeleka kilio hiki ingekuwa bora waziri wa elimu akalisemea hili na siyo vibaya Raisi wetu Jakaya M Kikwete akaingilia kati
 

Hii ni aibu kubwa kwa Taifa letu
 

Mungu



Maoni

Daaah, kwa kweli wanaoandika Matusi katika mitihani ni kuonyesha kabisa ni walikuwa wanafunzi wasio na nidhamu.. Wengi wao ndo wasumbufu kipindi wakiwa shuleni. Ni bora Sheria ijaribu kuwamulika hawa watu



Maoni

Mi naona elimu inashuka pamoja na takwimu kuonekana,hivyo serikal ingetafuta mafunzo maalum kwa wanaofanya vizur katika aidha masomo machache na kushindwa kuendelea,mf,kuna mtu ana b ya hesabu halafu masomo mengine amefel.