Thursday, October 20, 2011

Nyaraka za siri toka Vatican kuoneshwa hadharani, Februari, 2012 mjini Roma

 chanzo cha HABARI>>>www.radiovaticana.org
Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne, tarehe 5 Julai, 2011 ameongoza jopo la viongozi waandamizi kutoka Vatican wakati wa kuwasilisha mkakati wa Vatican kushiriki katika onesho la Kumbu kumbu za Nyaraka za Siri za Vatican, litakalofanyika kwenye Jumba la Makumbusho la Jiji la Roma, hapo mwezi Februari, 2012.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa nyaraka za siri kutoka nje ya Vatican kwa ajili ya onesha la hadhara. Mkutano na waandishi wa Habari umehudhuriwa pia na Mstahiki Meya wa Jiji la Roma, Giovanni Alemanno na ujumbe wake.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Kardinali Bertone anasema kwamba, tukio hili si la kawaida kwani linafanyika nje ya kuta za Vatican na litafanyika kwenye Jumba la Makumbusho la Roma, kitovu cha Jiji la Roma na utajiri wake unaofumbata uhusiano wa pekee na Vatican miaka nenda miaka rudi. Changamoto iliyokuwa mbele yao ni ile ya kuhakikisha kwamba, utajiri mkubwa, uzoefu na mang'amuzi yaliyoko kwenye nyaraka za siri za Vatican yanakwenda sanjari na matarajio ya Jiji la Roma.

Kwa upande wake, Kardinali Raffaele Farina, Mkutubi mkuu wa Vatican, alifafanua kwamba, nyaraka za kipapa zinazohifadhiwa kwenye Jumba la Kumbu kumbu za Nyaraka za Siri za Vatican ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa zima. Kwa mara ya kwanza, watu mbali mbali wanaweza kuzisoma nyaraka hizi ili kujichotea utajiri uliomo.

Askofu Sergio Pagano, Katibu mkuu wa Nyaraka za Siri za Vatican anasema, onesho hili linapania kutoa mwanga na uelewa mpana zaidi kuhusu asili na yaliyomo kwenye nyaraka hizi za siri zinazohifadhiwa katika Kumbu kumbu za Siri za Vatican, ndiyo maana onesho hili limepewa jina katika lugha ya Kilatini "Lux in Arcana" "Mwanga katika bahari". Kuna mammilioni ya nyaraka mbali mbali za Kanisa kutoka Vatican, kati ya hizo zote, Maktaba ya Vatican imeamua kuonesha nyaraka mia moja kwa wakati huu. Hali hii inaonesha kazi kubwa inayopaswa kufanywa ili kuwezesha umati mkubwa kushuhudia na kujisomea nyaraka hizi za Siri kutoka Vatican.

Kati ya nyaraka zitakazooneshwa ni ile ya Baba Mtakatifu Gregory wa Saba aliyeishi kunako mwaka 1073 hadi 1085; Barua ya Baba Mtakatifu Clementi wa Saba kwa Mfalme Henri wa nane kuhusu mgogoro wa ndoa, iliyoandikwa kunako mwaka 1530. Bila shaka wengi wangependa kufahamu kilichoandikwa na Kanisa wakati wa mashitaka ya Galileo Galilei kunako mwaka 1616 hadi mwaka 1633.

Askofu Pagano anasema, kwa mara ya kwanza, umma utapata fursa ya kujionea, kujisomea na kujichotea utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Nyaraka za Siri za Vatican. Maendeleo ya teknolojia ya habari yatawawezesha watazamaji kuingia katika undani wa nyaraka hizi za kipapa na kufanya tathmini ya kina kuhusu mchango wake kwa maisha na utume wa Kanisa; katika masuala ya maisha, tamaduni, ujuzi na maarifa.

Mstahiki Meya wa Jiji la Roma Giovanni Alemanno anasema, Jiji la Roma linaona fahari kubwa kuweza kuwa ni mwenyeji wa onesho hili la pekee, hali inayoonesha uhusiano wa karibu kati ya Vatican na Jiji la Roma katika maisha ya kiroho na kimwili. Tukio hili ni kielelezo cha ushupavu na uwazi wa Vatican kuweza kuonesha nyaraka za Siri, nje ya kuta za Vatican. "Lux Arcana" hapo Februari, 2012, itakuwa ni fursa nyingine kwa mahujaji kujionea utajiri uliomo kwenye Nyaraka za Siri za Vatican na hija ya maisha ya mwanadamu: kiroho na kimwili.

1 comment:

  1. Hii itakuwa nafasi nzuri kwa watu mbalimbali kwenda kujionea nyaraka muhimu za kanisa

    ReplyDelete